Breaking News

IDADI YA WATANZANIA WANAO NUFAIKA NA BIMA YA AFYA IMEONGEZEKA NA KUFIKIA ASILIMIA 33.




Na Mwandishi Wetu.
Idadi ya wanachama wachangiaji wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeongezeka hadi kufikia  wanachama 873,012 mwezi Septemba 2018 kutoka wanachama 164,708 waliokuwa wameandikishwa  mwaka 2001/2002.

Idadi hiyo ni sawa na asilimia 33 ya watanzania wote ambapo serikali imeweka lengo la kufikia nusu ya watanzani wote yani asilimia 50.



Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha  taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mfuko huo kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Bungeni jijini Dodoma.
“Ongezeko hili limetokana na kanuni na misingi  inayotumika katika kuendesha utaratibu wa mfuko huu ikiwa ni pamoja na uchangiaji wenye usawa kwa kuzingatia viwango vya mshahara,usawa katika kupata huduma na ushiriki wa Serikali katika usimamizi kwa faida ya wanachama” alisema Waziri Ummy.

 Waziri Ummy amesema kuwa kwa upande wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), jumla ya kaya zilizojiunga hadi Septemba mwaka huu ni 2,220,953 ikiwa ni sawa na wanufaika wapatao 13,506,330 sawa na asilimia 25 ya watanzania wote’ kwa hiyo mifuko hii yote inatoa huduma kwa watu 17,656,697 sawa na asilimia 33 ya watanzania wote kwa mujibu  wa idadi ya makadirio ya watanzania kwa sasa.

Idadi ya wanufaika imeongezeka  kutoka 691,774  mwaka 2001/2002 hadi wanufaika 4,150,367 sawa na asilimia 8 ya watanzania wote” alisema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa mpaka sasa idadi ya wanachama wengi waliojiunga  asilimia 67 ni watumishi wa umma ambao wanajiunga kwa mujibu wa sharia.
Hata hivyo Waziri Ummy alisema mfuko unaendelea kutoa elimu na kubuni vifurushi mbalimbali vitakavyovutia wananchi wengi kujiunga na kufaidika  na mfuko ambapo utawawezesha wanachama wengi zaidi kujiunga hasa wale wa sekta isiyo rasmi na kujiwekea malengo ya kuwafikia watanzia asilimia 50 mwaka 2020.

“Mfuko umekamilisha uandaaji wa vifurushi vya michango na mafao kulingana na uwezo wa wananchi kulipia bima  ya afya,suala hili lipo katika hatua za mwisho kabla ya kuanza kwa utekelezaji”. Alisisitiza Waziri Ummy.

No comments