MTENDAJI MKUU BODI YA FILAMU AKALIA KUTI KAVU.
KATIBU MKUU Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Susan Mlawi ameagizwa ampangie kazi nyingine Mtendaji Mkuu wa
Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, Joyce Fisoo na ateue mtu mwingine kushika
nafasi hiyo.
Agizo hilo lilitolewa jana jioni
(Jumatano, Aprili 24, 2019) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akihitimisha
kikao chake na wasanii zaidi ya 100 kutoka Shirikisho la Filamu Tanzania
kilichofanyika Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.
Shirikisho la Filamu Tanzania
linajumuisha vyama 11, ambapo 10 vimesajiliwa na kimoja hakijakamilisha
usajili. Vyama hivyo ni vya waigizaji, waongozaji, watayarishaji, wahariri,
wachekeshaji na wapigapicha. Wengine ni waandishi wa miswada (script writers),
watafutaji mandhari, wasambazaji wa filamu, walimu na chama cha wanawake wa
tasnia ya filamu ambacho bado kiko kwenye mchakato wa usajili.
Kikao hicho ambacho kilidumu kwa
zaidi ya saa saba, kilihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bodi ya Filamu Tanzania pamoja na Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) wakiongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Juliana
Shonza.
“Katibu Mkuu mtafutie eneo jingine
la kufanya kazi. Hana tuhuma zaidi ya mahusiano mabaya na wadau wake, ana
historia nzuri, lakini tatizo ni mahusiano. Mpeleke idara nyingine na hapa
mlete mtu mwingine,” alisema Waziri Mkuu.
“Mama Fisoo wewe uko clean,
sina tatizo na utendaji wako lakini ukikaa hapa hutaweza kwenda mbele na wala
hawa wote hawatakuja kufanya kazi na wewe. Tunataka hii tasnia iende mbele,
tunataka maendeleo kwenye tasnia ya filamu,” alisisitiza Waziri Mkuu.
Alimuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya
Filamu Tanzania, Profesa Frowin Nyoni ajipange upya na Bodi yake na kuhakikisha
kuwa wanatoa elimu kwa wasanii kama ambavyo imeainishwa kwenye sheria ya
kuanzishwa kwa Bodi hiyo.
“Bodi yako inao wajibu wa kutoa
elimu kwa makundi tofauti ya wasanii. Sheria yenu imeainisha kuwa mnapaswa
kutoa elimu. Wapeni refresher courses ili waongeze ujuzi na
wakienda huko wanatoa uzoefu walionao kwa wanachuo, nao pia wanakuwa
wamejifunza,” alisema.
“Nimeangalia makundi ya wasanii na
kukuta kuna wachoraji na wachongaji; wasanii wa filamu, wasanii wa maigizo,
wabunifu wa mitindo na wote hawa wana Bodi zao. Timizeni majukumu yenu. Bodi
pia mna kazi ya kupromote brand kwa kutumia wasanii wetu,”
alisema.
Kuhusu utitiri wa tozo ambao
umelalamikiwa na wasanii hao, Waziri Mkuu alisema kuna haja ya kulinda soko la
ndani la kazi za wasanii wa Kitanzania tofauti na hali ilivyo sasa ambapo
wazawa wanatumia gharama kubwa kutengeneza kazi zao lakini wanapata shida
kuziuza ilhali wageni wanapata faida zaidi kwa kazi kama hizo.
“Wasanii wamesema kuna tozo 11
lakini Mtendaji Mkuu kataja tozo chache tu. Hebu Waziri aitishe kikao baina
yenu, Waziri wa Fedha, Waziri wa Viwanda na Biashara, Kamishna wa TRA, Bodi ya
Filamu na TCRA, mkutane mara moja na kuziangalia upya hizi tozo ili zipunguzwe
kama tulivyofanya kwingine. Lazima tulinde soko la ndani,” alisisitiza.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia
fursa hiyo kuwaonya wasanii juu ya fukuto linaloendelea ndani kwa ndani baina
ya vyama tofauti, baina ya vyama na shirikisho na baina ya shirikisho na
taasisi nyingine za kiutendaji.
Kuhusu maudhui ya filamu
zinazotengenezwa na wasanii wa Tanzania, Waziri Mkuu alisema inashangaza kuona
masuala ya mapenzi yanaongoza kwenye filamu za Kitanzania kwa kushika nafasi ya
kwanza ikiwa ni sawa na asilimia 68, ikifuatiwa na vichekesho ambayo inashika
nafasi ya pili ikiwa sawa na asilimia 12.
“Je, wote ni lazima muigize masuala
la mapenzi kwenye filamu zenu au huwa mnaambiana mtoe maudhui yanayohusu
mapenzi. Je, ni kweli kwamba Watanzania wengi wanapenda kuangalia mambo ya
mapenzi?”
“Ni lazima muangalie maudhui yenu na
mpanue wigo. Kwa kuwa mna shirikisho, ni vema mkagawana maeneo ya kuigiza ili
kupanua soko na mkiingiza filamu zenu sokoni, zote zipate mashabiki.”
Alisema nafasi ya tatu kwenye
maudhui imechukuliwa na filamu za masuala ya utamaduni na mambo ya uchawi
ambayo ni sawa na asilimia 10 huku nafasi ya nne ikichukuliwana na filamu
zinazohusu mapigano ambazo ni sawa na asilimia saba. “Hizi ni chache kwa sababu
zinahitaji mtaji mkubwa wakati wa kuzitengeneza na pia ni risky,”
alisema.
Wakitoa maoni yao ni kwa nini tasnia
ya filamu imedidimia, wasanii hao ambao waliwakilisha wenzao kutoka mikoa ya
Tanga, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro, Geita, Katavi na Rukwa, walidai
kwamba Bodi ya Filamu imeua tasnia hiyo kwa hiyo hawana imani na Bodi na hawako
tayari kufanya nayo kazi.
Waliomba pia kuwe na taratibu za
kuvutia wawekezaji kwenye tasnia hiyo, uwekwe mkakati wa haraka wa kuinua soko
la filamu kupitia lugha ya Kiswahili ambayo walisema ni bidhaa adimu. Pia
waliomba sera ya filamu nchini ikamilishwe haraka ili iweze kulinda maslahi ya
wasanii wa filamu.
No comments