Breaking News

SURUA TISHIO LA AFYA ZA WENGI DUNIANI.

Mtaalamu wa chanjo toka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt William Mwengee

Na. Melkiory Gowelle.

Imeelezwa kuwa dhana ya kudharau chanjo imesababisha kurejea kwa baadhi ya magonjwa ikiwemo Surua ambayo kwasasa imekuwa tishio kwa afya za watu wengi ulimwenguni ambapo barani Afrika asilimia 700%  ya watu wanaathiriwa na ugonjwa huo.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es salaam na mtaalamu wa chanjo toka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt William Mwengee, amesema nchi ya Ukrain ni kinara kwa maambukizi Duniani wakati Afrika Taifa la Demokrasia ya Kongo linashika namba moja kwa mlipuko wa ugonjwa huo.

Kuhusu Tanzania Mwengee amesema nchi hiyo imepiga hatua katika kutokomeza ugonjwa wa Surua, hivyo Wananchi wake hawatakiwi kujisahau sababu chanjo ni muhimu, waendelee kuithamini ili kuboresha afya zao juu ya magonjwa ya mlipuko.

"Surua imerudi kwa kasi sana ambapo imeanza kuleta athari kubwa tokea mwaka jana lakini Tanzania imekuwa ni moja kati ya nchi chache zilizo katika kiwango cha chini cha maambukizi ya Surua na Lubela ambapo kwa mwaka jana kuliripotiwa watu 74 tu walioambukizwa.”amesema Mwengee.

Aidha Mwengee amewataka Wanahabari kutumia taaluma yao kuwasisitiza watanzania kuthamini na kuhudhuria chanjo za Magonjwa yote.

“Lazima tusisitizane ili tuchanje, kama nchi kubwa duniani zimeathiriwa vipi sisi Tanzania.? Hatutakiwi kulala kwani tukifanya hivyo tutaumia sana.” Amesisitiza Mwangee.

Kwa upnde wake Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo toka Wizara ya Afya Dr. Dafrossa Lyimo ameelezea dhamira ya Chanjo kuwa ni kupunguza vifo ambapo kila dose moja inapunguza vifo millioni 10.6, hivyo ni muhimu kwa atakaye anza Chanjo kufuatilia ratiba kama aina ya chanjo hiyo inavyotaka.

“Ni muhimu sana kukamilisha ratiba ya chanjo ili kuepuka kurudi wodini kutibiwa kutokana na kupata magonjwa hasa ya mlipuko.” Ameeleza Dr Lyimo.

Amesema kwa sasa Wizara kupitia Idara ya Chanjo nchini  inatoa jumla ya Chanjo tisa zinazokinga magonjwa  13 na dhamira kuu ya idara hiyo ni kumfikia kila anayestahili kupata chanjo mahali popote kwa usawa.

Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo toka Wizara ya Afya Dr. Dafrossa Lyimo

Katika hatua nyingine Mtaalamu wa Chanjo kutoka idara hiyo Dkt. Lotalis Gadau ameelezea kuhusiana na tatizo kubwa linalo wasumbua akina mama la Saratani ya mlango wa kizazi ambapo Wanawake elfu 50, wanapatwa na tatizo hilo kila mwaka.

Amesema ni idadi inayotishia amani na ametaja sababu kubwa ya kufikia idadi hiyo ni dhana potofu inayoenezwa na Watu wengi kuwa Chanjo ya HPV inayokinga Saratani hiyo inazuia akina mama kupata ujauzito.

“Saratani hii ndio Saratani pekee inayoongoza kwa madhara makubwa na chanjo yake inatolewa kwa mabinti wa miaka 14, hivyo waachane na uvumi, waende kwenye vituo vya afya kupata chanjo ili kuepuka madhara.” Amesisitiza Gadau.

Idara ya Chanjo kwasasa inaadhimisha wiki ya chanjo iliyoanza tarehe 22 mwezi huu na kumalizika tarehe 30 ambapo inatekeleza mikakati mingi ya kupunguza vifo ili kufikia malengo yake.

No comments