Breaking News

MBUNGE MATTEMBE APEWA TUZO MAALUM


Na Mwandishi wetu
UONGOZI wa Sekondari ya Mwanamwema Shein, wazazi na wanafunzi wamemkabidhi tuzo na cheti cha utendaji kazi bora katika jamii kwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuboresha miundombinu shuleni na kuwezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu.

Mattembe ambaye alifanya ziara shuleni hapo kujionea mazingira ambapo hakuridhishwa kuona wanafunzi wa kike wa kidato cha tano wakilala chini na kuleta vitanda vyenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 40 kwa wakati mmoja na kukabidhi kwa uongozi wa shule.

Hata hivyo, kukabidbiwa kwa vitanda hivyo ni mwendelezo wa jitihada binafsi za Mattembe kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali shuleni hapo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo na cheti Maalumu cha shukrani, Mkuu wa Sekondari ya Mwanamwema Shein, Zainabu Mtinda amesema Mattembe amekuwa akifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wake wanasoma katika mazingira salama na tulivu.

"Amekuja hapa mara kadhaa na kila anapokuta mambo tofauti anarudi na ufumbuzi wake, ameshatuletea vitu mbalimbali na leo ametuletea vitanda 20 vya double decker, huu ni msaada mkubwa sana na wanafunzi wetu wataondokana na changamoto ya kulala kwenye mikeka.

"Tumewaza sana ni kitu gani tutakupa ili kukutia moyo, wazazi na wanafunzi wakasema hii tuzo na cheti kitakuwa ukumbusho wa miaka mingi kwani, kila ukikitazama utakumbuka hiki kikubwa ulichotupatia. Tunakushukuru sana na tu akuombea kwa Mungu azidi kukubariki," alisema Mwalimu huyo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Singida, Eliah Digha alimpongeza Mattembe kwa kujitoa kwa ajili ya wananchi wa Singida na moyo huo unapaswa kuigwa na wabunge wengine.
Aliwataka wanawake na vijana kuendelea kumtumia mbunge huyo na kumpa ushirikiano wa hali na mali kwa kuwa anaana dhamira njema na wananchi na sio mtu wa kujali maslahi na tumbo lake kama wengine.


"Jamani mnanijua vizuri sana, lakini naomba kuwaeleza ukweli hapa kuwa huyu Mattembe ndio mtu wa kumshika mkono. Anahudumia mkoa mzima bila upendeleo. Leo utasikia ametoa msaada na kufanya ziara Ikungi, kesho Mkalama mara yuko Iramba na hawa ndio watu tuliokuwa tunawataka. Hana makundi wala husikii fitna kwa huyu ni kazi kazi tu," alisema Digha.

Mbali na kukabidhi vitanda hivyo, Mattembe pia alitembelea kituo cha afya cha Mgori na kukabidhi msaada wa mashuka 50 na vifaa tiba ili kusaidia uboreshaji wa huduma za afya.

No comments