WAZIRI MKUU AFUNGUA MAFUNZO KWA WAKUU WA MIKOA NA MA’RAS * ASEMA MAFUNZO HAYO YATAWASAIDIA KUSIMAMIA UTUMISHI NA KUZINGATIA MIIKO YA UONGOZI.
WAZIRI Mkuu,
Kassim Majaliwa, akifungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala
wa Mikoa kwenye ukumbi wa Hazina Jijni Dodoma, leo Desemba 3, 2018. (Picha zote na Ofisi
ya Waziri Mkuu).
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amefungua mafunzo kwa wakuu wa mikoa
na makatibu tawala wa mikoa, ambapo amesema baada ya mafunzo hayo
Serikali inatarajia watasimamia kikamilifu nidhamu katika utumishi wa umma na
wao wenyewe watakuwa kioo katika kuzingatia miiko ya utumishi wa umma.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema viongozi
hao wa mikoa watazingatia kikamilifu mipaka ya madaraka yao na kwamba hatua
watakazozichukua katika uongozi na utendaji wao zitazingatia sheria, kanuni na
taratibu zilizopo nchini.
Waziri Mkuu alifungua mafunzo hayo
yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi leo Desemba 3, 2018 katika ukumbi wa
Hazina Jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wakasimamie
kikamilifu mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.
“Mkadumishe uhusiano mwema baina yenu na watumishi walio
chini yenu, kwa kuzingatia kuwa kila mtumishi anao mchango katika kuboresha
utendaji kwenye kituo chake cha kazi. Nina matarajio makubwa kuwa mtadumisha
uhusiano mzuri kikazi na viongozi wa juu na pia uhusiano wa diplomasia ya
heshima na viongozi wengine ndani ya mihimili yetu mitatu,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao wahakikishe kila
mmoja wao anaandaa mpango kazi unaoainisha shughuli zake za kila siku. “mkuu wa
mkoa, katibu tawala wa mkoa, mkuu wa
wilaya na mkurugenzi na wakuu wa idara
wote na watumishi wote wawe na mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu yao,”
alisisitiza Majaliwa.
Alisema viongozi hao wanatakiwa wasimamie nidhamu kazini na
uwajibikaji wa watumishi kwa wananchi, ambapo pia amewasihi watende haki kwa
wananchi na watumishi walio chini yao. Pia lazima watumishi wa serikali
wawapokee na kuwahudumia wananchi kwa staha, wawasikilize kero zao na
kuzitafutia ufumbuzi.
BAADHI ya Makatibu Tawala wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, (hayupo pichani) wakati alipofungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
BAADHI ya Makatibu Tawala wa Mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, (hayupo pichani) wakati alipofungua Mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwenye Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Waziri Mkuu alisema viongozi hao wanatakiwa waendelee kusimamia
amani na utulivu kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila
wasiwasi wowote kwani amani na utulivu ndiyo itawawezesha nchi
iendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.
“Tunakumbushwa sisi viongozi tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali
za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote bila kubagua jinsia, kabila, dini,
rangi ya ngozi, mtu atokako ndani ya nchi ilimradi hajavunja sheria wala
ubaguzi mwingine wa aina yoyote. Tunaaswa tuwahudumie Watanzania
wote kwa usawa,” alisema.
Kuhusu mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo, Majaliwa alimesema zitawawezesha viongozi hao
kupata fursa ya kutafakari na kujitathmini kuhusu hatua za kujiimarisha zaidi
kiuongozi na kiutendaji. “Hatua hizo ni lazima ziwe pamoja na kubadilika
kwa mtazamo na kujirekebisha endapo mtabaini maeneo mliyokuwa mkikosea tangu
mlipokabidhiwa ofisi hadi sasa.”
Kwa mujibu wa Majaliwa, mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo
zinahusu majukumu na mipaka ya kazi, ambapo watajifunza namna ya kufanya
kazi bila mikwaruzano isiyo na tija baina yao na viongozi wa mihimili mingine
ya dola, viongozi wa kisiasa na watendaji wengine serikalini.
Alisema mada nyingine inahusuuongozi,
hisia na mahusiano mahali pa kazi, ambapo itawawezesha kujiimarisha katika
mbinu za kuwaongoza watumishi walio chini yao kwa kujenga na kudumisha
mshikamano na ushirikiano wa pamoja.
“Mada itafafanua pia namna mnavyotegemeana
na watumishi wa kada na ngazi mbalimbali katika kutimiza majukumu yenu. Ni
muhimu sana kufanya kazi kama timu moja ili muweze kuyafikia malengo ya taasisi
kwa upana wake na si malengo ya mtu au kiongozi mmoja,” alifafanua.
Alisema kwenye mada inayohusu muundo wa Serikali na namna
inavyofanya kazi watauelewa vizuri zaidi muundo wa huo ulivyo na jinsi
unavyofanya kazi.
Pia, wataielewa vizuri zaidi itifaki na kuheshimiana kwa ngazi
mbalimbali kuanzia ya waziri, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, makatibu tawala, wakurugenzi,
wakuu wa idara hadi wananchi.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph
Semboja, alisema mafunzo hayo ya wiki moja yatajikita katika maeneo
makuu matatu ambayo ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika kufanya maamuzi ya
kimkakati yanayozingatia mahitaji na manufaa mapana ya sasa na ya baadae kwa
jamii.
Alitaja eneo la pili kuwa ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika
kuongoza rasilimali watu na kusimamia rasilimali nyingine ili kutekeleza kikamilifu
na kwa mafanikio maamuzi ya kimkakati waliyoyafanya katika kipengele cha
kwanza.
“Eneo la tatu ni la kuimarisha uwezo wa washiriki katika
kujijengea sifa binafsi za uongozi ili awe na ushawishi kwa wananchi
anaowaongoza. Hili ni jambo la msingi, kiongozi mwenyewe awe mfano bora wa
kuigwa. Awe muadilifu, mtenda haki, mfuata sheria na taratibu pamoja na
kufahamu na kuheshimu miiko ya uongozi,” alisema.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, Mkuu wa mkoa wa Dodoma,
Dk. Binilith Mahenge na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat
Kandege, pamoja na maofisa wengine wa serikali.
No comments