Breaking News

WEKEZENI KWENYE VIWANDA UMEME BORA, WA UHAKIKA UPO-MHANDISI MANDA.



MENEJA Miradi (Uzalishaji) wa Shirika la Umeme nchini, (TANESCO), Mhandisi Stephene Manda, akiwa kwenye chumba cha udhibiti mitambo cha Kituo hicho leo Januari 9, 2019.  
                                Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Umeme Nchini (TANESCO) limewahimiza wananchi kuwekeza kwenye viwanda kwakuwa hivi sasa umeme bora na wa uhakika upo.

Wito huo umetolewa leo Januari 9, 2019 Jijini Dar es Salaam na Meneja Miradi wa Shirika hilo, anayeshughulikia uzalishaji (Generation) Mhandisi Stephene Manda.
Mhandisi Manda, alikuwa akielezea utekelezaji wa miradi ya umeme Kinyerezi II wa Megawati 240 na ule wa upanuzi wa Kinyerezi I wa Megawati  185.

 “Mradi wa Kinyerezi namba II wa Megawati 240 umekamilika, kwa hiyo ombi letu kwa wote ambao wanaweza kuwekeza kwenye viwanda wawekeze kwani umeme wa uhakika na wa kutosha  upo.” Alisema.
Manda alisema kuwa, licha ya mradi huo wa Kinyerezi II, mradi mwingine ni wa upanuzi wa Kinyerezi I unaozalisha megawati 150 ili ufikie Megawati 335 kwa kuongeza Megawati 185.

“Itakapofika Agosti 2019 jumla ya umeme utakaokuwa unatoka Kinyerezi pekee ni Megawati 575 kwa hivyo ni umeme wa kutosha  upo.
Kama ni kulisha Jiji la Dar es Salaam, basi Kinayerezi inaweza kutosha na kwa kupata umeme wa uhakika.” Alisema.

 MUONEKANO wa kituo cha kufua umeme wa gesi Kinyerezi II cha Jijini Dar es Salaam, kama kinavyoonekana katika picha ya dron iliyopigwa mwishoni mwa Desemba 2018. Kwa mujibu wa Meneja Miradi (Uzalishaji) wa Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO), Mhandisi Stephene Manda, kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 240 kimekamilika.

Meneja huyo aliwahakikishia wenye viwanda kuwa uwezo wa kuwahudumia upon a kwamba TANESCO imejipanga vizuri na kuwaomba wawekezaji wawekeze.

Alisema hakuna ulazima kwa wawekezaji kuwa na viwanda vikubwa, bali hata kwa vile vidogo kama vile vya kukoboa na kusaga nafaka na vile vya kukamua matunda vitahudumiwa.
 
Manda alitoa  wito kwa Watanzania kuuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wake Rais Dk. John Magufuli, kujenga uchumi wa kati na wa viwanda kwani inawezekana kwa vile umeme wa uhakika upo na ni bora zaidi.

No comments