Breaking News

MKOPO WA MASHARTI NAFUU KUMALIZA TATIZO SUGU NCHINI.


SERIKALI ya Tanzania leo J’4 March 5, 2019 imesaini mikataba miwili ya mikopo na Benki ya Maendeleo Afrika yenye thamani ya shilingi za kitanzania Bilioni 589.26 kwaajili ya ujenzi wa barabara inayo sababisha adha ya usafiri kwa kipindi kirefu ya Kabingo-Kasulu-Manyovu Kigoma, yenye urefu wa kilomita 260 kwa kiwango cha lami .

Zoezi hilo limefanyika leo Jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Doto James akiwakilisha Serikali ya Tanzania na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika Alex Mubiru na kushuhudiwa na maafisa wa Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa Maendeleo Afrika.

Akizungumza katika hafla hiyo Doto ameishukuru Benki ya maendeleo Afrika kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za uwekezaji katika miundombinu ya Usafiri kwa kuwapa mikopo wa Masharti nafuu zaidi.

“Mradi huu ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya awamu ya tano ambao unalenga uimarishaji wa miundombinu ya usafiri ili kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kupunguza umasikini na kuimarisha ushirikiano wa Kikanda.” Amesema Doto

Ameeleza kuwa Barabara hiyo ni kiunganishi muhimu  katika maendeleo na uboreshaji wa biashara ndani na nje ya nchi hivyo utakwenda sambamba na ujenzi wa Barabara ya Rumonge-Gitaza (km45) nchini Burundi ili kuboresha mtandao wa barabara za Afrika Mashariki.

“Barabara hii itakapokamilika itaunganisha Bandari ya Dar es salaam na Mikoa ya Magharibi mwa Tanzania  na kufungua Masoko ya kikanda nchini Burundi, Rwanda, Uganda na Jmhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.” Amesema Doto.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkazi wa Benki ya Maendeleo Afrika Alex Mubiru ameipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kuchochea kasi ya maendeleo kiuchumi hivyo wao kama wadau wa maendeleo wapo tayari kuunga mkono Jitihada hizo.

“Kwa niaba ya Benki ya maendeleo Afrika napenda kuthibitisha ahadi yetu ya kuwasaidia watu naSerikali ya Tanzania katika jitihada zao za kutambua matarajio yao kuwa Nchi ya Uchumi wa kati hivi karibuni.” Amesema Mubiru.

No comments