Breaking News

OIE KUINUA SEKTA YA MIFUGO NCHINI


Kikao cha ana kwa ana kati ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Abdallah Hamis Ulega  (wa pili kutoka kulia) na Uongozi wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE). Kutoka kushoto: Mwakilishi wa OIE Kanda ya Kusini mwa Afrika Samuel Wakusama, Rais wa OIE na Kamisheni ya Australia  Mark Schipp na Mkurugenzi Mkuu wa OIE Monique Eloit na Mkurugezi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (wa kwanza kulia) Hezron Nonga.


 NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega ameliomba Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) kuisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto zinazoikabili katika sekta ya mifugo ambazo zinasababisha  nchi kushindwa kusafirisha mifugo na mazao yatokanayo na mifugo kama vile nyama kwenda katika masoko ya nje ya nchi.

Maombi hayo yamewasilishwa leo nchini Tunisia ambapo Naibu waziri Ulega amehudhuria Mkutano Mkuu wa 23 wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) Kamisheni ya Afrika, uliofanyika Mjini Hammament nchini humo.
Mara baada ya mkutano huo, Ulega akiambatana na Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa wizara hiyo Hezron Nonga amepata fursa ya kufanya kikao cha ana kwa ana na uongozi mkuu wa Shirika hilo la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) kwa kuzungumza na rais wa shirika hilo Mark Schipp, Mkurugenzi Mkuu Monique Eloit na mwakilishi wa shirika hilo kwa Ukanda wa Nchi za Kusini mwa Afrika Samuel Wakusama.
Ulega ameziainisha changamoto hizo kuwa ni pamoja na magonjwa, kasi ndogo ya mifugo kuzaliana (Poor Breeding) na uzalishaji duni (Low Productivity) ambapo kwa pamoja uongozi huo umeahidi kuzifanyia kazi.
Mkutano huo uliojumuisha nchi zaidi ya 25 za bara la Afrika zikiwemo Zambia, Zimbabwe, Misri, Kenya, Uganda, Tunisia na Chad ulikuwa na malengo ya kuangalia afya ya wanyama, haki za wanyama, uzalishaji wa mifugo na usalama wa chakula kitokanacho na mifugo na kutoa mapendekezo kulingana na kanuni za shirika hilo duniani.
Katika mazungumzo hayo, Ulega ameshukuru uongozi huo kwa ushirikiano wake na Tanzania kwa kuendelea kuisaidia nchi katika miradi mbalimbali ya kulinda afya za wanyama hapa nchini.
Licha ya mazungumzo hayo, Ulega kupitia kwa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Hezron Nonga, amewakabidhi andiko linalofafanua kwa kina sekta ya uvuvi nchini, changamoto zake na maeneo yenye uhitaji ili kuuwezesha uongozi huo kuendelea katika hatua ya utekelezaji.
Pamoja na mambo mengine, Ulega ameueleza uongozi wa OIE kuhusu nia ya Tanzania kuandaa mkutano ujao kwa kuwa ni nchi yenye mifugo na wanyamapori wengi, mazingira mazuri ya uwezekaji na taasisi maalum zinazoshughulikia masuala ya viwango, ubora wa bidhaa na usalama wa chakula.
Katika kutathmini afya za wanyama, wataalamu wamejadili magonjwa mbalimbali ya wanyama yaliyopo katika bara la Afrika hususan kwa nchi wanachama, athari na namna yakuyakabili yakiwemo magonjwa ya miguu na midomo (FMD), Kichaa cha mbwa na homa ya Bonde la Ufa (RVF).
Aidha kikao kimetathmini kwa pamoja miradi mbalimbali yenye lengo la kuimarisha afya za wanyama pamoja na michango ya wahisani ikiwemo Benki ya Dunia, Mchango wa Wataalam wa Kati wa Mifugo (Veterinary Paraprofessionals) na nafasi yao katika kuimarisha huduma za afya ya wanyama katika Bara la Afrika.


No comments