TUME YA UCHAGUZI HAIWEZI KUSIMAMAIA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA - MAJALIWA
* Asema
si jukumu lake kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiwezi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
kama ambavyo imependekezwa na baadhi ya Wabunge.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo
(Jumanne, Aprili 9, 2019) Bungeni jijini Dodoma, kwenye mkutano wa 15 wakati
akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa
Bunge kwa mwaka 2019/2020.
Amejibu hoja iliyotolewa kwamba Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa usisimamiwe na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na badala yake usimamiwe na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Pia waliitaka Serikali ishughulikie jambo hilo
mapema ili kuepuka usumbufu unaoweza kutokea.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Waziri
Mkuu alisema Serikali inawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa imani kubwa
walioionesha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ni huru, juu ya utekelezaji
wa majukumu yake, na kuona umuhimu wa kuiongezea jukumu la kusimamia Uchaguzi
wa Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, Majaliwa alisema,
majukumu ya Tume hiyo, yameainishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kusimamia Uchaguzi wa Rais, Wabunge
na Madiwani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Hivyo, jukumu la kusimamia uchaguzi
wa Serikali za Mitaa si miongoni mwa majukumu ya Tume kwa mujibu wa Katiba,”
alisema.
Katika
hatua nyingine, akizungumzia kuhusu uwekezaji
kwenye zao la pamba, Waziri Mkuu alisema sekta ya pamba na mnyororo wake
wote wa thamani ni sekta ya kipaumbele ambayo mbali na kuwahakikishia soko
wakulima na kuongeza kipato chao, uwekezaji katika viwanda vya nguo
unatengeneza ajira nyingi kwa vijana hivyo kuinua kipato chao na kuboresha
maisha ya watu wengi.
“Kwa kutumia mkakati wa kuzalisha
nguo na mavazi mbalimbali (Cotton to Clothing - C2C), Serikali
itaendelea kuhamasisha
uwekezaji wa viwanda kwa kutumia teknolojia za kisasa za kutengeneza nguo
kuanzia kuchakata pamba hadi nguo kwa kuhakikisha kuwa taratibu zote
zinafanyika nchini na msisitizo uwe kwenye utengenezaji wa nyuzi,” alisema.
Amejibu hoja
iliyotolewa kwamba bado zao la pamba halijatumiwa vizuri katika kuongeza pato la Taifa na
kuinua maisha ya Watanzania. Pia Wabunge walitaka Serikali ijizatiti
kusimamia uwekezaji kwenye kilimo cha zao la pamba ili kufanikisha utekelezaji
wa mkakati wa viwanda vya nguo nchini wa kufikia malengo ya kuwa Taifa lenye
uchumi wa kati.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta
binafsi mwaka 2017, ilifanya tathmini ya kina na kuandaa Blueprint ambayo
imebainisha masuala yote muhimu yanayokwamisha uwekezaji na kuainisha maeneo
yote muhimu yayohitaji kurekebishwa ikiwemo sheria, kanuni na taratibu
zinazosimamia uwekezaji nchini kwa kila taasisi.
Alikuwa akijibu hoja kuhusu umuhimu
wa Serikali kufanya tathmini na kuangalia vikwazo vinavyokwamisha harakati
za uwekezaji nchini, kutunga sheria mpya, kurekebisha baadhi ya sheria ili
kuendana na mahitaji ya Blueprint.
Alisema sambamba na hatua hiyo, huduma
zimeimarishwa kwa kuanzisha mifumo ya kielektroniki ambapo wawekezaji wataweza
kufanya maombi ya vibali mbalimbali wakiwa popote bila kulazimika kufika
kituoni.
“Mifumo hii itaondoa urasimu na
kuharakisha utoaji wa vyeti vya uwekezaji, leseni na vibali mbalimbali. Hatua
hizi zitapunguza gharama na muda wa mwekezaji kufuatilia vibali na leseni kwa
kila taasisi,” alisema.
Alisema, Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC) hivi sasa kina ofisi saba za kanda ambazo ni Mwanza, Dodoma,
Moshi, Kigoma, Mtwara, Mbeya na Dar es Salaam ambazo zimeanzishwa kwa lengo la
kusogeza huduma karibu na wawekezaji.
Bunge lilikubali kupitisha sh. 148,886,523,581/-
kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka
2019/2020. Kati ya hizo, sh. 86,290,355,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya
kawaida na sh. 62,596,168,581/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile, Bunge liliidhinisha sh.
124,182,537,600 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo sh.
116,573,026,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 7,609,511,600/- ni
kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
No comments