Breaking News

ESRF, UNICEF WAKUTANA NA SERIKALINI KUPATA UFUMBUZI WA CHANGAMOTO ZA WATOTO NA VIJANA MAENEO YA MIJINI.

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria warsha hiyo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa warsha hiyo ya kujadili namna ya kutatua changamoto za watoto mtoto na vijana katika majiji na miji, warsha iliyofanyika jijini Dodoma tarehe 11 Septemba 2019.

Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

KATIKA kuhakikisha changamoto za watoto na vijana maeneo ya Mijni zinapatiwa ufumbuzi, jana tarehe 11 Septemba 2019 Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na UNCEF, kupitia Maabara ya Ukuaji wa Miji Tanzania (TULab), wamewakutanisha wadau na wataalam kutoka serikalini kujadiliana namna ya kumlinda mtoto hasa maeneo ya mijini.

Akizungumza wakati wa Warsha  hiyo Mkuu wa Idara ya Utafiti Mkakati na Machapisho kutoka ESRF, Profesa Fortunata Makene, amesema lengo  la kukutana kwa wadau hao ni kupata maoni yatakayosaidia kuanzisha programu itakayosaidia kutatua changamoto za watoto na vijana ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mtoto analindwa.

Kwa kuweka mazingira mazuri katika majiji na miji.
Amesema warsha kama hii iliofanyika Dodoma itafanyika pia Mikoa ya Dar es saalam na Mbeya, ambapo watakutana na wadau kutoka Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s), Sekta Binafsi pamoja na watoto wenyewe.

Amesema washiriki wa warsha ya leo ni wataalam zaidi ya 20 kutoka serikalini yaani  TAMISEMI, Ofisi ya Takwimu, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, Chuo Kikuu cha Dodoma nk., wote hawa wakiwa ni wadau wa ukuaji wa miji. 

Ilielezwa katika kupanga miji ni lazima mipango hiyo iwe rafiki kwa watoto ili isiweze kuwaathiri, amesema watoto wamekuwa wakiathiriwa sana na ukuaji wa miji na hata wengine kujiingiza katika mambo ambayo yanawaathiri na kushindwa kufikia malengo yao.

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa katika miji ambazo zimekuwa zikiwaathiri au kuathiri ukuaji  kwa watoto ni pamoja na ajira za watoto, hii imetajwa kuwa ni changamoto ambayo imekuwa ikiathiri watoto kwa sababu watoto wengi wamekuwa wakijiingiza katika kutafuta kipato kujikimu.

Upatikanaji wa maji hasa kwa maeneo ambayo hayajapimwa imekuwa ni changamoto kwa sababu watoto ndio huenda kutafuta maji na huko ndio hukutana na vitendo ambavyo huwaathiri katika ukuaji wao kwa matukio ya ukatili.

Mitandao ya kijamii pia imetajwa kama ndio chanzo cha watoto wa mijini kuathiriwa katika ukuaji wao tofauti na watoto wa vijijini, pia wadau wameshauri kuendelea kutoa  elimu kwa watoto ili waepukane na athari hizo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Watoto kutoka wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mwajuma Magwiza, amesema serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwamo kuanzisha dawati la watoto.  

Pia uanzishwaji wa huduma ya simu kwa watoto kupitia namba 116, ambayo mpaka sasa imesaidia kusikilizwa kwa mashauri 43 ya watoto yakijumuisha ubakaji, mimba na ndoa za utotoni, Pia wamefanikiwa kutoa huduma muhimu kwa watoto 329 wanaoishi kwenye vituo vya
kulelea watoto.

Mgeni rasmi katika warsha hii alikuwa Dr. John K. Jingu, Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, ambaye aliwakilishwa na Mwajuma Magwiza, Mkurugenzi, Maendeleo ya  watoto.

No comments