Breaking News

JPM AISHUKURU CHINA KWA UHUSIANO NA USHIRIKIANO MZURI, NI KATIKA MAKABIDHIANO YA MAGARI 40 YA JWTZ.


Rais Dkt. John Magufuli amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping kwa kuuendeleza ushirikiano na uhusiano mzuri wa Tanzania na China ikiwemo misaada na uwekezaji ambao China inaufanya hapa nchini.

Rais Magufuli ametoa shukrani hizo leo tarehe 12 Septemba, 2019 katika hafla ya makabidhiano ya magari 40 kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) kwenda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyofanyika katika Makao Makuu ya JWTZ Upanga Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amesema pamoja kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii, ulinzi na usalama na miundombinu, China ndio nchi inayoongoza kwa uwekezaji hapa Tanzania ikiwa na miradi 723 yenye thamani ya takribani shilingi Trilioni 13.581 na iliyozalisha ajira 87,126.

Ametaka uhusiano huo uimarishwe zaidi kwa JWTZ na PLA kujenga kiwanda kikubwa chenye uwezo wa kubangua tani laki 2 za korosho kwa mwaka, jambo ambalo litasaidia kuongeza thamani ya korosho za wakulima wa Tanzania na kupelekwa China ambako kuna mahitaji makubwa ya korosho.

Amemuomba Lut. Jen. Shao Yuanming aliyeiwakilisha PLA katika makabidhiano ya magari hayo na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke kufikisha shukrani zake kwa Rais Xi Jinping kwa kuuendeleza na kuukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri wa Tanzania na China na pia kufikisha ombi la kujengwa kwa kiwanda hicho.

Ameishukuru China kwa kutoa msaada wa magari hayo 40 kwa JWTZ ambayo amesema yataimarisha utendaji kazi wa jeshi hilo na pia ameomba PLA isaidie upatikanaji wa ndege kubwa za kubebea Askari na vifaa kwa ajili ya jeshi hilo.

“Makabidhiano haya ya magari 40 ni kielelezo kingine tena cha uhusiano wa karibu, kidugu na kirafiki uliopo kati ya Mataifa yetu mawili, tunaishukuru sana China kwa misaada mbalimbali iliyoitoa kwa Tanzania.”

“China imekuwa mdau mkubwa wa biashara kwa nchi yetu na pia inasaidia katika utalii, kwa mfano mwaka huu tunatarajia kupata watalii 10,000 kutoka China” amesisitiza Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Lut. Jen. Shao Yuanming amemshukuru Rais Magufuli kwa kuhudhuria tukio hilo na kwa kuundeleza na kuukuza uhusiano wa Tanzania na China ukiwemo uhusiano wa kijeshi na ameahidi kuwa PLA itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na JWTZ.

Nae Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo ametaja baadhi ya maeneo ambayo JWTZ imenufaika kutokana na ushirikiano wake mzuri na PLA kuwa ni pamoja na kujengwa kwa Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi huko Mapinga Wilayani Bagamoyo kilichogharimu shilingi Bilioni 67, ukarabati na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Ngerengere uliogharimu shilingi Bilioni 137.63.

Ujenzi wa awamu ya 2 ya Chuo cha Ulinzi wa Taifa Mkoani Dar es Salaam (NDC) utakaogharimu shilingi Bilioni 57 na kwamba kwa sasa PLA inakamilisha maandalizi ya kujenga Makao Makuu ya JWTZ Mkoani Dodoma na kushirikiana na JWTZ katika zoezi kubwa la kijeshi litakalofanyika hapa nchini kwa lengo la kubadilishana ujuzi katika ulinzi na usalama.

Jen. Mabeyo amemuomba Lut. Jen. Shao Yuanming kufikisha shukrani za JWTZ kwa uongozi wa juu wa PLA kwa msaada wa magari hayo 40 na misaada mingine inayotokana na ushirikiano wa majeshi hayo.

Pia, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuagiza JWTZ ipatiwe magari makubwa 12 yaliyokuwa yakitumiwa na Bodi ya Dawa (MSD) ili yasaidie shughuli za jeshi.



No comments