DKT. NDUGULILE : FUATILIENI MTOTO ALIYEKATWA MKONO MWANANYAMALA.
Naibu
Waziri Dkt. Faustine Ndugulile akiwa kwenye picha ya pamoja na bodi mpya ya
nane ya baraza la maabara binafsi za afya.
Na. Catherine Sungura –Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee wa Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amemuagiza Msajili
wa Baraza la Madaktari la Tanganyika kushirikiana na Baraza la Wauguzi na
Wakunga Tanzania kufuatilia mtoto aliyekatwa mkono baada ya kuhamishiwa
hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa ya
Mwananyamala.
Dkt. Ndugulile ametoa maagizo
hayo wakati akizindua bodi ya nane ya maabara binafsi za afya kwenye ukumbi wa
Veta jijini hapa.
“Nilitegemea baraza la madaktari
muwe mmeanza uchunguzi, kwahiyo nakupa maagizo kesi hiyo muanze kufuatilia na
kama itathibitika ni uzembe waliohusika wachukuliwe hatua, ndani ya wiki mbili
mtuletee majibu ili mimi na Waziri tujue tunachukua hatua gani.
Dkt. Ndugulile amesema kwenye
mabaraza bado kuna changamoto ya baadhi ya mashauri kuchukuliwa hatua hivyo
kama mabaraza ya kitaakluma ni vyema kuangalia ufanisi wa majukumu yao na
kuchukulia hatua pale taaluma inapokosewa na waliokosea wachukuliwe hatua.
Dkt. Ndugulile ameitaka bodi hiyo
kusimamia usajili wa maabara zote nchini kwani hivi sasa imetokea uanzishwaji
wa maabara kiholela zinazotoa huduma kwa wananchi bila ya kusajiliwa hivyo
kufanya ukaguzi ili kubaini maabara hizo na kuzichukulia hatua.
“Naomba sheria ifuate mkondo wake
ili kubaini wale wote walioanzisha huduma za maabara bila kufuata sheria na
taratibu za usajili, tushirikiane kuhakikisha kuwa hakuna taasisi au mtu
atakayefungua au kutoa huduma za maabara bila kusajiliwa”. Amesisitiza Dkt.
Ndugulile.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema
baraza hilo ni chombo muhimu na ndio moyo wa sekta ya afya kwani maabara inatoa
muelekeo wa mgonjwa kwa kuthibitisha tatizo, hivyo inahitajika maboresho katika
utoaji huduma za maabara.
“Sasa hivi huduma hizi zimekua ni
biashara kwani asiliamia 70 ya homa wala sio Malaria ni virusi watu wanakunywa
dawa sana pasipo kuzingatia misingi kwani maabara hizi zinatumika kama sehemu
ya matibabu na hata upasuaji, mtu anaenda maabara anakaa dakika kumi na tano
anaambiwa ana UTI wakati mwingine anaambiwa ana malaria plasi plasi hii maana
yake ni nini hili linahitaji ufuatiliaji”. Alisema Dkt. Ndugulile.
Hata hivyo aliitaka bodi hiyo
mpya kusimamia ubora wa huduma za maabara ili kuinufaisha jamii na
kuhakikisha huduma za afya katika jamii zinaboreshwa kukidhi viwango
vitavyotarajiwa na hivyo kuboresha afya na maisha ya watanzania.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Baraza
la maabara binafsi Prof. Said Abood aliahidi kutekeleza maagizo yote
waliyopewa na Naibu waziri ikiwemo ya kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili
kubaini maabara bubu na ambazo hazijasajiliwa pamoja na kuhakikisha
maabara zinatoa huduma zinazostahili ili kuweza kumsaidia daktari kumpatia
mwananchi huduma stahili.
No comments