TOZENI BILI ZA MAJI ZISIZOWAUMIZA WANANCHI-MAJALIWA.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji ifuatilie
utendaji wa Mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maji katika
maeneo mbalimbali nchini na ihakikishe kwamba bili wanazotozwa wananchi
zinakuwa na uhalisia na si kuwaumiza.
Ametoa agizo hilo baada ya kuibuka wimbi la malalamiko kutoka kwa
wananchi kuhusu upandaji wa bili za maji ambao hauna uhalisia kwa sababu
Serikali ndiyo inayotoa fedha za miradi hiyo nchini.”Serikali haitakubali wala haitoruhusu
mwananchi anatozwa gharama kubwa za maji.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 12, 2019) Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbungewa Viti Maalumu, Mariam Kisangi, aliyetaka kujua kauli ya Serikali
kuhusu suala hilo.
“Yako maeneo ambayo mamlaka zilizopewa dhamana ya kusimamia miradi
ya maji kumejitokeza wimbi la mabadiliko ya kuhusu kupanda kwa bei za bili,
mfano wilayani Maswa mkoani Simuyu bei imeongezeka kutoka sh. 5,000 hadi 28,000
kwa mwezi.”
“Bei hizo hazina uhalisia na hakuna sababu ya mamlaka kuzoza bei
kubwa kiasi hicho na kuwafanya wananchi washindwe kumudu kulipia bili zao,
wakati Serikali ndio imetoa fedha za kugharamamia uanzwishwaji wa miradi hiyo
na haijadai kurudishiwa fedha hizo.”
Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maji kupitia
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ifuatilie bei za bili
wanazotozwa wananchi ili kujiridhishwa kwamba zinazingatia uwezo wa wananchi
wengi kuzilipa hasa wale wa vijijini.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya,
Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Kilimo na Maafisa Biashara kote nchini
wasimamie katika masoko yote na wajirishe iwapo vipimo vinavyotumika ni sahihi
kwani lumbesa haikubaliki.
Ametoa
agizo hilo wakati akijibu swali la Mbungewa Jimbo la Mlalo, Rashid
Shangazi aliyetaka kupata kauli ya Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika
kudhibiti unyonyaji wanaofanyiwa wakulima kupitia ufungaji wa mazao unaozidi
viwango.
Waziri Mkuu amesema
wanunuzi wa mazao mbalimbali lazima wafuate sharia, kanuni na taratibu za
manunuzi ya mazao husika. “Maafisa Kilimo wasimamie biashara hiyo na waendeshe
operesheni kwenye maeneo ya masoko ili kujirishana vipimo vinavyotumika.”
Amesema ni muhimu zaidi kutumia mizani ambayo haina utata ili
kuwawezesha wakulima kuweza kunufaika kutokana na kilimo na kwamba suala la
waununuzi kutumia vipimo visivyosahihi kama lumbesa halikubaliki.
Akijibuswali
la Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa aliyetaka kupata kauli ya Serikali kuhusu
kuhusu suala la ununuzi wa zao la pamba, Waziri Mkuu amesema Serikali
imelifanyia kazi suala hilo na tayari zaidi ya tani 200,000 zimeshanunuliwa
ambayo ni sawa na asilimia 80.
Waziri Mkuu amewahakikishia wakulima wa zao la pamba kwamba
pamba yote iliyosailia majumbani itanunuliwa.
No comments