TUME YA UTUMISHI WA WALIMU PAMOJA NA WALIMU4,046 WAFUKUZWA KAZI
Naibu Waziri (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwita Waitara akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa kazi wa Makatibu wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu wa Wilaya, Tanzania Bara. Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo jijini Dodoma, Novemba 26 na 27, 2019.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Bibi Winifrida Rutaindurwa akitoa maneno ya kumkaribisha mgeni rasmi (Naibu Waziri - TAMISEMI, Mhe. Mwita Waitara) katika mkutano wa kazi wa Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu wa Wilaya, Tanzania Bara
Baadhi ya Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu wakiwa wanamkaribisha mgeni rasmi (hayupo pichani) katika ukumbi wa Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo jijini Dodoma
Naibu Waziri (Elimu), Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwita Waitara (katikati mwenye tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Walimu pamoja na wageni waalikwa kutoka Chama cha Walimu Tanzania, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo katika mkutano wa kazi wa Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu kutoka Wilaya za Tanzania Bara.
Baadhi
ya Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu wakiwa katika hali ya
utulivu wakati wa mkutano wa kazi uliofanyika Novemba 26 na 27, jijini Dodoma.
Dodoma
Katibu Ofisi ya Rais,
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutaindurwa amesema jumla ya walimu
4,046 wa shule za msingi na sekondari wamefukuzwa kazi kutokana na makosa
mbalimbali yakiwemo utoro kazini, kukiuka maadili na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi.
Rutaindurwa ameyasema
hayo jana katika mkutano wa siku mbili uliolenga kuwajengea uwezo
Makatibu Wasaidizi wa TSC kutoka Wilaya zote Tanzania Bara uliofanyika katika
ukumbi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, jijini Dodoma.
Katika Maelezo ya
kumkaribisha Naibu Waziri (Elimu) wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe.
Mwita Waitara, Rutaindurwa alisema kuwa tangu TSC ianze kufanya kazi mwezi
Julai, 2016 walimu 7,123 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu baada ya kukiuka
maadili ya kiutumishi.
“Mheshimiwa Naibu Waziri katika makosa yaliyotendwa kwa kipindi
cha miaka mitatu, makosa 5,447 yalikuwa ya utoro kazini, makosa 1,290 kukiuka
maadili, makosa 162 uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi na makosa mengine kwa
ujumla wake yalikuwa 224”, alieleza Rutaindurwa
Alifafanua kuwa TSC imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za
kiutumishi kwa mujibu wa Sheria Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Walimu ambapo
walimu 4,046 walifukuzwa kazi, walimu 930 walipewa onyo/karipio,
walimu 284 walipunguziwa mshahara, walimu 244 walisimamishiwa
nyongeza ya mshahara, walimu 237 walishushwa cheo na walimu 14 walipewa adhabu
ya kufidia hasara.
Alieleza kuwa walimu wengi walikutwa na makosa ya utoro wakati wa
zoezi la uhakiki wa watumishi kwa kuwa waliondoka kwenye vituo vyao vya kazi
bila kufuata taratibu na kuruhusiwa na waajiri wao, hivyo walichukuliwa hatua
za kinidhamu.
“Wengi wa walimu waliotiwa hatiani kwa makosa ya utoro, walikuwa
wameenda masomoni bila kupata ruhusa kutoka kwa waajiri wao na zoezi la uhakiki
wa watumishi lilipofanyia ndipo ikagundulika kuwa ni watoro na mchakato wa
kuwachukulia hatua za nidhamu ukaanza,” alisema.
Akifungua Mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
TAMISEMI, Naibu Waziri anayeshughulikia elimu katika ofisi hiyo, Mhe. Mwita
Waitara alieleza kuwa TSC bado ina kazi ya kufanya ili kuhakikisha walimu
wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya taratibu za kiutumishi ili wajiepushe na
makosa ya kinidhamu.
Aliweka bayana kuwa Serikali haijivunii kuwafukuza kazi walimu
wake iliyowaajiri yenyewe ikizingatiwa kuwa bado kuna changamoto ya upungufu wa
walimu katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kwa kweli tunasikitika kuwa idadi ya walimu waliofukuzwa kazi ni
kubwa, lakini ni lazima watumishi wa umma muelewe kuwa Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli haina huruma kabisa na
watumishi wazembe wasiozingatia Maadili na Miiko ya kazi yao”, alisema Mhe.
Waitara.
Pamoja na hayo, Mhe. Waitara alieleza kuwa walimu wamekuwa na kero
na malalamiko mbalimbali yanayosababishwa na kutowajibika kikamilifu kwa baadhi
ya watendaji wa wanaoshughulikia masuala yao.
Alieleza baadhi ya kero hizo kuwa ni kucheleweshwa kwa malipo ya
kusafirisha mizigo kwa walimu waliostaafu, walimu waliostahili kupandishwa
madaraja kutopandishwa kwa wakati, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
kukataa kupitisha barua za walimu wanaoomba kuhama kutoka Wilaya moja kwenda
nyingine na walimu kutotendewa haki katika mashauri ya nidhamu.
Kutokana na changamoto
hizo, Naibu Waziri alipiga marufuku tabia ya baadhi ya Wakurugenzi wa Mamlaka
za Serikali za Mitaa ya kuzuia kupitisha barua za walimu wanaoomba uhamisho na
kueleza kuwa wao sio wenye mamlaka ya kutoa uamuzi wa ombi la mwalimu anayetaka
kuhamia wilaya nyingine.
“Ni marufuku kwa
Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzuia kupitisha barua za walimu
wanaoomba uhamisho. Wao wanapaswa kupitisha, kuweka maoni yao na kuruhusu
maombi hayo yaende kwa mhusika aliyeandikiwa. Mwenye mamlaka ya kukubali au
kukataa ombi la uhamisho wa mwalimu ni Katibu Mkuu, TAMISEMI,”
alisisitiza Mhe. Waitara.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri
aliiagiza TSC kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuandaa orodha
ya walimu waliostahili kupandishwa madaraja lakini hawakupandishwa na kuiwasilisha
TAMISEMI ili taratibu nyingine ziweze kufanyika.
No comments