WAZIRI MKUU, KASSIM MAJALIWA AKAGUA MIRADI WA NYUMBA ZA NSSF, ZILIZOPO TUANGOMA KATIKA WILAYA YA KIGAMBONI, JIJINI DAR ES SALAAM
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi
wa NSSF, Balozi Alli Siwa, wakati
alipokagua Miradi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Taifa na Shirika la Nyumba la
Taifa ya Ujenzi wa nyumba Tuangoma, Mtoni Kijichi na Dungu, Novemba 27, 2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wakati alipotembelea mradi wa nyumba za NHC, zilizopo Mtoni Kijichi katika Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Novemba 27, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akioneshwa jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wakati akikagua mradi wa nyumba za NSSF, zilizopo Tuangoma katika Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Novemba 27, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wakati akikagua mradi wa nyumba za NSSF, zilizopo Tuangoma katika Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam, Novemba 27, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua
mradi wa nyumba za Watumishi Housing, uliyopo Dege wilayani Kigamboni, jijini
Dar es Salaam, Novemba 27, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
27, Novemba, 2019
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
NSSF, NHC, WHC KAMILISHENI MIRADI YA NYUMBA KIGAMBONI -MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema nyumba zote zinazojengwa na Taasisi za Umma katika wilaya
Kigamboni jijini Dar es salaam zinapaswa kukamilika haraka ili ziuzwe ua
kupangishwa kama ilivyokusudiwa.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Novemba 27,
2019) baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba za NSSF, NHC na Watumishi
Housing iliyopo katika wilaya ya Kigamboni.
Waziri Mkuu amesema
inasikitisha kuona kwamba watumishi wa umma na wananchi jijini Dar
es Salaam hawana nyumba nzuri za kuishi wakati zipo nyumba
nyingi nzuri zimejengwa na zinahitahi umaliziaji mdogo tu ili ziweze
kukalika.
Hivyo, Waziri Mkuu ameitaka Menejimenti ya
NSSF kakamilisha haraka ujenzi na uwekaji wa miundombinu ya umeme, maji safi na
maji taka katika nyumba zake 161 zilizoko Tuangoma, 820
zilizoko Mtoni Kijichi na 439 zilizoko Dungu ili ziuzwe na kuepusha uwezekano
wa uharibifu unaoweza kutokea kwa nyumba hizo kakaa muda mrefu bila
kupata wanunuzi au wapangaji.
Ili kufanikisha jambo hilo Mheshimiwa
Majaliwa amemtaka Mthamini Mkuu wa Serikali atathimini nyumba hizo na
kutoa bei halisi ya soko kwa sasa ili kuwawezesha Watanzania
wengi na hasa watumishi wa Umma kununua na kupanga katika nyumba hizo.
Pia, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa
wilaya na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigamboni kuwasaidia
watumishi wa wilaya na Halmashauri hiyo kuingia mikataba rafiki
itakayowawezesha watumishi hao kupewa kipaumbele katika kununua au kupanga
kwenye nyumba hizo.
Mheshimiwa Majaliwa pia ameitaka
Menejimenti ya NSSF kufikiria namna ya kuzungumza na viongozi wa vyuo
mabalimbali kama vile Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Mwalimu
Nyerere ili wanafunzi wa vyuo hivyo wapatiwe fursa ya kupanga katika nyumba hizo
kwa bei watakazomudu.
Pia Mheshimiwa Majaliwa ameuagiza uongozi
wa Mkoa wa Dar es salaam ukishirikiana na SUMATRA kuanzisha njia za
mabasi ya daladala zitakazoanzia au kupitia kwenye nyumba za NSSF
Mtoni Kijichi na Dungu ili kuwezesha wapangaji na wananchi watakaonunua nyumba
hizo kupata usafiri wa umma.
Vilevile, Waziri Mkuu ameuagiaza uongozi
huo kuhakikisha kwamba eneo la Mtoni Kijichi zilipojengwa nyumba za NSSF na NHC
linapata huduma za Shule, Kituo cha Afya na Kituo cha Polisi kwani litakuwa na
wakazi wengi .
Ili kuongeza thamani ya nyumba hizo na
kuvutia wapangaji na wanunuzi, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Menejimenti ya NSSF
kuboresha barabara kwenye mitaa yote zilipojengwa nyumba hizo kwa kushirikiana
na TARURA.
“Nashauri ziwekwe taa za sola kwenye
barabara za mitaa yote ya nyumba hizi ili kupendezesha eneo na kuwafanya
wananchi wahamasike kununua na kuishi katika nyumba hizi” amesema Majaliwa.
Akiwa kwenye Mradi wa Nyumba za NHC Mtoni
Kijichi, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea Shule ya Awali ya Kids
Paradise na kufurahishwa na utaratibu mzuri wa shirika hilo wa kukumbuka
kujenga jengo zuri la Shule hiyo na kulipangisha ili kuhakikisha
kwamba watoto wanaoishi katika nyumba hizo wanapata fursa ya kusoma
elimu ya awali.
Akizungumza baada ya kukagua Mradi wa
ujenzi wa nyumba za NHC Mwongozo, Mheshimiwa Majaliwa ameutaka uongozi wa
NHC kuwa karibu na wateja wanaopanga au kununua nyumba zao. “
Shughulikieni malalamiko yote yanayotolewa na wateja wenu ili
wajenge imani kwenu, Alisisitiza Majaliwa.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama alisema wizara yake
imeyapokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu na kwamba watafanya kila
njia ili kuhakikisha kwamba majengo yote yanakamilika haraka na kuuzwa au
kupangishwa.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya makazi, william Lukuvi alimwambia Waziri Mkuu kuwa amekwishatoa
maagizo kwa NHC ijenge uzio japo wa waya na wapande michongoma ili
kuweka ulizi kwenye eneo la nyumba zao za Dungu.
Mheshimiwa Lukuvi alisema amewapa NHC
miezi mitatu ili wafanye marekebisho katika nyumba ambazo zimelalamikiwa na
wateja kuwa zina kasoro ili kujenga imani kwa wateja wao.
Mapemba Mkadiriaji Majengo wa NSSF, Abon
Mhando ambaye pia ni Kaimu Meneja wa Miradi wa NSSF
alimwambia Waziri Mkuu kuwa Mradi wa ujenzi wa nyumba wa
Tuangoma una jumla ya nyumba 161 na kati ya hizo nyumba 76
zimekamilika. Aliwataja wakandarasi wanaojenga mradi huo kuwa ni Kampuni za
CASCO, Advent na NANDRA.
Alisema Mradi wa Dungu una
jumla ya nyumba 439 na kati ya hizo nyumba 95 zimekamilika na jumla ya
makampuni 13 yameshiriki katika ujenzi wa mrdi huo.
Kuhsu mradi wa Mtooni
Kijichi Mhando alisema mradi huo una jumla ya nyumba 820
na kati ya hizo nyumba 417 zimekamilika.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, NOVEMBA 27, 2019.
No comments